Rungu la ECOWAS laiangukia Mali

0
178

Viongozi wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) 
wameisimamisha Mali uanachama, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika wiki iliyopita, yakiwa ni ya pili ndani ya kipindi cha miezi 9.

Kiongozi wa Mapinduzi hayo ambaye kwa sasa ndiye Rais wa mpito wa Mali Kanali Assimi Goïta,  ni miongozi mwa Viongozi wa nchi Wanachama wa ECOWAS walioshiriki katika mkutano uliofanyika mjini Accra nchini Ghana ambapo uamuzi huo umefikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, – Shirley Ayorkor Botchwey amewaambia Waandishi wa habari mjini Accra kuwa Viongozi wa ECOWAS wameiagiza Mali kuchagua Waziri Mkuu wa kiraia haraka iwezekanavyo.

Mali pia imeagizwa kuhakikisha inaitisha uchaguzi wa Rais baada ya kukamilika kwa kipindi cha uongozi cha mpito ambacho ni miezi 18.

Rais wa Mpito wa Mali Kanali Assimi Goïta aliingia madarakani wiki iliyopita baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kulazimisha kukamatwa kwa Rais Bah Ndaw ambaye naye alikuwa ni wa mpito pamoja na Waziri Mkuu wa nchi  hiyo Moctar Ouane.