Rugemalira aomba kesi yake ifutwe Mahakani

0
170

Na,Emmanuel Samwel TBC

Jamhuri imeomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali hoja za mawakili wa utetezi katika Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washitakiwa James Lugemalira na wenzake wawili ambao wameomba kufutwa kesi inayowakabili wateja wao.

Kauli hiyo imetolewa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon baada ya jopo la mawakili linalowatetea Rugemalira kudai mahakama hiyo inaweza kutumia mamlaka yake kufuta kesi hiyo kwa kuzingatia vipengele vya sheria, kauli iliyopingwa na Simon.

“Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi kama hii, ama DPP mwenyewe atoe mamlaka kwa mahakama hii hivyo naomba mahakama yako isiingizwe chaka kwani hoja tuliyotoa ni ya msingi sana na suala la ‘plea bagain’ ni la pande zote mbili yaani DPP na Jamhuri,” amesema Wakili Simon.

Kuhusu hoja ya makubaliano ya awali Simon amedai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka na Upande wa Jamhuri haijatoa kauli rasmi na kwamba suala la ‘plea bargaining’ ni la majadiliano na kubainisha kuwa yanaendelea na iwapo itashindikana mahakama hiyo itajuzwa.

Awali, upande wa utetezi uliwasilisha hoja mbele ya mahakama hiyo ikiomba shauri hilo kufutwa kwa madai kuwa ni mwaka wa tano sasa tangu shauri hilo lilipofikishwa mahakamani na kwamba hakuna maendeleo yoyote yanayoendelea juu ya shauri hilo.

Na kuhusu hoja ya ‘Plea bargain’ na hoja ya siku kumi na tano za nyongeza zilizotolewa na Hakimu Shaidi mawakili hao wamesema mahakama iliamuru DPP awafuate washitakiwa hao kwakuonesha nia ya kuonana na DPP ikiwa ni pamoja na kuwasilishwa vielelezo vinavyoonyesha ushahidi.

Kwa Upande wake Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Huruma Shaidi amesema ni kweli washitakiwa wamefuata utaratubu kama inavyotakiwa lakini upande wa DPP haujawa wazi kukubali au kukataa kukutana na DPP kwa mujibu wa sheria.

“kwenye kesi hii nilitoa siku 40 Upande wa Jamuhuri kuja na majibu yanayoeleweka lakini hakuna kinachoendelea na kwamba kila mtu anatakiwa aongozwe kwa hekima kwakuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na si vinginevyo”Amesema Hakimu Shaidi.

Hata hivyo kesi hiyo imehairishwa hadi Mei 6 mwaka 2021 itakapotajwa tena na washitakiwa wamerudishwa rumande.