Venezuela imeonesha mkanda wa video inayomuonesha mmoja wa askari mamluki raia wa Marekani ambaye ni miongoni mwa askari 13 waliokamatwa baada ya kushindwa kwa shambulio la kigaidi.
Katika video hiyo Luke Daenman amekiri kuwa katika shambulio lililokuwa limepangwa aliagizwa kuuteka Uwanja wa Ndege wa Caracas kisha ipelekwe ndege itakayomchukua Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro baada ya kumteka na kumpeleka Marekani.
Mbali na Daenman, mamluki wengine waliokamatwa wamedai kutumwa na Jordan Goudreau ambaye ni Mkuu wa Kampuni ya Kijeshi ya SilverCorp USA yenye makao yake Mjini Florida, Marekani.
Goudreau ambaye alikuwa askari wa Marekani ameviambia vyombo vya habari kwamba kampuni yake imewaajiri askari mamluki wawili raia wa Marekani kutekeleza operesheni ya kumteka na sio kumuua Rais Maduro.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo na Bunge la Congress wameagiza uchunguzi ufanyike dhidi ya Goudreau ambaye pia anachunguzwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara haramu ya silaha.
Kwa upande wake Rais Maduro amelaani vikali jaribio hilo huku akiituhumu Marekani na Colombia kwa kuhusika, tuhuma ambazo Rais wa Marekani, Donald Trump amezikanusha.
Maduro amekuwa akiituhumu Colombia ambayo inashirikiana na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi kwa kuendesha harakati za chini kwa chini za kumuondoa madarakani na kisha kumweka mpinzani wake, Juan Guaido.