Rais Trump amuomba radhi Jaji Kavanaugh

0
2044

Rais Donald Trump wa Marekani amemuomba radhi kwa niaba ya raia wa nchi hiyo, Jaji mpya wa Mahakama Kuu Brett Kavanaugh kwa kile alichokiita ni kampeni chafu za kisiasa zilizolenga kuharibu sifa zake kwa kumsingizia mambo ya uongo.

Trump ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe za kuapishwa kwa Jaji Kavanaugh, sherehe zilizofanyika katika Ikulu ya Marekani.

Mchakato wa kumthibitisha Kavanaugh katika uteuzi wake, uligubikwa na kashfa za udhalilishaji anaodaiwa kuufanya mwaka 1980.

Rais Trump amewaeleza watu walioshuhudia sherehe za kuapishwa kwa  Kavanaugh kuwa tangu awali alisikia madai kutoka chama cha Democratic kupinga uteuzi wa Jaji huyo ambaye binafsi amemuita kuwa ni mtu makini na ambaye hana jambo lolote baya alilolifanya, na kwamba madai hayo ni jitihada za kutaka kumchafua.

Kauli hiyo ya Rais Trump ameitoa wakati wa kiapo hicho ambacho ni cha awali kwa Kavanaugh kilichosimamiwa na Jaji wa mahakama Kuu anayemaliza muda wake Anthony Kennedy huku akiwa amebakiwa na kiapo cha mwisho kutoka kwa Rais.