Rais Samia ahimiza SADC kutengeneza chanjo ya UVIKO-19

0
478

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa mataifa yaliyoendelea kuongeza muda wa ulipaji wa mikopo kutokana na uchumi wa mataifa mengi ya Afrika kuathiriwa sana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19).

Rais Samia ametoa rai hiyo wakati akitoa hotuba ya kujitambulisha kwenye Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ulioanza leo jijini Lilongwe nchini Malawi.

Ameongeza kuwa kutokana na janga hilo kuendelea kuisumbua dunia, njia pekee ya kupunguza athari za janga hilo ni kutoa chanjo kwa wananchi wa SADC.

Aidha amesema kuwa mahitaji ya chanjo ni makubwa kuliko usambazaji, hivyo ametoa wito kwa mataifa wanachama wa SADC kushirikiana ili kutengeneza chanjo na vifaa tiba, na kuyashawishi makampuni yanayotengeneza chanjo kutoa ujuzi ili chanjo hizo zitengenezwe katika maeneo mengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi amesema kuwa hakuna nchi itakayosema iko salama hadi pale mataifa yote yatakapokuwa salama, hivyo ushirikiano ni muhimu katika kukabiliana na athari za UVIKO-19.