Papa Francis awasili Iraq, ziara ya kihistoria

0
262

Papa Francis amewasili Baghdad nchini Iraq kwa ziara ya siku nne na kuweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa Katoliki kuzuru taifa hilo.

Ziara hiyo itagusia masuala mbalimbali yakiwemo vita, amani, umasikini na mgogoro wa kidini katika eneo hilo la Mashariki ya Kati.

“Nina furaha kusafiri tena,” amesema Papa Francis wakati akizungumza na wafuasi wake akiondoka kuelekea Iraq, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu janga la corona lilipoikumba dunia.

Awali wakati kukiwa na msisitizo kuwa asisafiri alisema kuwa Wakristo nchini Iraq hawastahili kuangushwa kwa mara ya pili baada ya Papa John Paul II kufuta safari yake mwaka 1999 wakati mazungumzo kati yake na serikali ya Rais Saddam Hussein yalipovunjika.

Miongo miwili tangu hapo idadi ya Wakristo nchini humo imepungua kutoka waumini milioni 1.4 hadi kufikia 250,000 ikiwa ni asilimia 1 ya raia nchini humo.

Wengi wamekimbia nchini humo kukwepa vurugu ambazo limekuwa likiighubika taifa hilo tangu mwaka 2003.

Takribani maafisa usalama 10,000 wa Iraq wametengwa kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa kiongozi huyo ambapo pia zuio la watu kutotoka nje limewekwa ili kudhibiti maambukuzi ya COVID19.