Papa Benedict azikwa Vatican

0
236

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ameongoza ibada ya mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVI katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya sasa, Papa aliyeko madarakani ndiyo ameongoza Misa Takatifu na kuhubiri katika mazishi ya mtangulizi wake.

Maelfu ya waombolezaji wamejitokeza mapema Alhamisi asubuhi katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuhudhuria mazishi ya mwanatheolojia huyo wa Ujerumani.

Kengele ziligongwa na umati wa watu ulipiga makofi wakati ambapo jeneza lenye mwili wa Benedict lilipitishwa kutoka sehemu lililpokuwa limewekwa ndani ya kanisa na kulihamishia mbele ya altare iliyo mbele ya viwanja hivyo, huku makadinali waliovalia mavazi mekundu wakitazama.

Papa Mstaafu Benedict XVI, hakuwa tena kiongozi wa Taifa, lakini viongozi mbalimbali duniani, akiwemo Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz na Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni wamehudhuria mazishi yake.

Mwili wa Benedict umezikwa katika kaburi ambalo mwili wa Papa John Paul II ulizikwa kabla ya kuhamishwa kwa ajili ya kutangazwa kuwa Mwenye Heri mwaka 2011. Makaburi hayo ya kipapa yako chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.