Pakistan yashutumiwa kwa mlipuko wa bomu

0
1037

Serikali ya India imesema kuwa itafuata taratibu zote za Kidiplomasia kuwafikisha katika vyombo vya sheria Wanamgambo wote waliohusika na mlipuko wa bomu uliosababisha vifo vya watu 46 katika jimbo la Kashmir upande wa India.

India  inaishutumu Pakistan kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya Wanamgambo wa kikundi cha Jaish-E-Mohammad ambao wamekua wakifanya mashambulio ya mara kwa mara.

Katika taarifa yake, Serikali ya India imetaka kuungwa mkono na nchi mbalimbali ili kuwawekea vikwazo Wanamgambo hao na imetaka kiongozi wao Masood Azhar kuorodheshwa kama Gaidi katika rekodi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

India imedai kuwa, mara kwa mara imetaka kuchukuliwa hatua kali kwa Wanamgambo hao wa kikundi cha Jaish-E-Mohammad, lakini imekua ikipata kikwazo kutoka China ambayo ni mshirika wa Pakistan.

Mlipuko huo katika jimbo la Kashmir upande wa India  ulilenga msafara wa askari wa jeshi la India uliokuwa ukielekea kwenye doria.