NJAA YASABABISHA KULA WADUDU

0
225

Madagascar inaelekea kuwa nchi ya kwanza duniani kuingia katika baa la njaa kutokana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa, tayari maelfu ya watu nchini humo wameathirika na njaa kutokana na ukosefu wa mvua kwa muda wa miaka minne mfululizo.

Ukame ambao ni mbaya zaidi ndani ya kipindi hicho cha miaka minne iliyopita, umeathiri jamii za Wakulima zilizojitenga kusini mwa nchi hiyo ukiacha familia zikitafuta wadudu kama chakula.

“Hizi ni hali za njaa na zinatokana na mabadiliko ya Tabianchi na si mapigano.” Amesema afisa wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Shelley Thakral.

Umoja Wa Mataifa unakadiria kuwa watu elfu 30 nchini Madagascar wapo hatarini kutokana na kukosekana kwa chakula, na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kasi kutokana na nchi hiyo kuanza kuingia katika majira ya ukame.

“Hili halikutazamiwa, hawa watu hawajafanya chochote kibaya kuchangia mabadiliko ya Tabianchi lakini bado ndio wanaathirika na mabadiliko hayo.” ameongeza Thakral.

Mabadiliko ya Tabianchi yanatabiriwa kuathiri uchumi wa dunia katika miaka michache ijayo, ambapo chuo cha Re cha nchini Switzerland kimetabiri kuwa asilimia 18 ya pato la Taifa duniani kote itapotea kabla ya mwaka 2050 kutokana na mabadiliko ya Tabianchi.