Waziri Mkuu wa Israel,- Benjamin Netanyahu amekanusha madai ya ufisadi dhidi yake na kusema kuwa ataendelea na majukumu yake kama kawaida licha ya kufunguliwa mashtaka.
Netanyahu amekanusha madai hayo baada ya Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, – Avichai Mandelblit kumfungulia mashtaka ya kupokea rushwa, udanganyifu na kuvunja uaminifu.
Mwenyewe Netanyahu amesema kuwa, hatua hiyo ya kufunguliwa mashtaka ni njama za kisiasa na pia ni jaribio jaribio la Mapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Israel, amemfungulia mashtaka Netanyahu katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa pamoja na uwezekano wa kufanyika uchaguzi kwa mara ya Tatu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, baada ya Netanyahu na hata aliyekuwa mpinzani wake Benny Gantz kushindwa kuunda serikali.
