Nchi za SADC zatakiwa kuungana kumaliza ugaidi Msumbiji

0
176

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) ambaye pia ni Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera amesema changamoto za kiusalama nchini Msumbiji ni changamoto za Jumuiya nzima, kwa kuwa matishio ya usalama nchini humo yanaweza kuziathiri nchi nyingine za SADC.

Dkt. Chakwera ametoa kauli hiyo mjini Lilongwe nchini Malawi, wakati akifungua mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali wa SADC.

Amesema nchi za SADC zinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha matukio ya kigaidi yanakomeshwa nchini Msumbiji na kuhakikisha amani inarejea nchini humo baada ya kuwepo kwa matukio kadhaa ya kigaidi.

Hata hivyo Rais Chakwera amezishukuru nchi zinazochangia vikosi vyake katika misheni ya SADC iliopo nchini Msumbiji, kwa kuendelea kujitolea licha ya changomoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa UVIKO – 19.

Rais Chakwera amesema nchi za Kusini mwa Afrika zimekua pamoja wakati wa kupigania uhuru, zimekua pamoja katika wakati wa majanga mbalimbali ya asili pamoja na changamoto za maradhi, hivyo hazina budi kuwa pamoja sasa kuhakikisha ugaidi unakwisha nchini Msumbiji.

Katika mkutano huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali wa SADC umepokea na kujadili taarifa ya mkutano wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya siasa, ulinzi na usalama
,Jamhuri ya Msumbiji na nchi zinazochangia vikosi katika jeshi la utayari la SADC lililopo nchini Msumbiji uliofanyika tarehe 11 Januari Llilongwe Nchini Malawi.