Wakati dunia ikiendelea kuomboleza kifo cha nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani, Kobe Bryant, bintiye Gianna pamoja na watu wengine saba, nabii mmoja kutoka nchini Ghana amesema kuwa anaweza kufuta masikitiko hayo kwa kumfufua Bryant na mwanae.
Nabii Nigel Gaisie amesema hayo wakati akizungumza na kuwashuhudia waumini wake juu ya kile anachodai kuoneshwa na Mungu na kwamba Mungu amemuamuru kumrejesha nyota huyo wa NBA.
“Mungu alinichukua katika ulimwengu wa roho, na nikaona mwisho wa mtu mashuhuri. Taarifa hizi zitaitikisa dunia kutokana na namna mtu huyo alivyo mkubwa. Nimeona watu wengi sana kwenye mitandao ya kijamii wakimzungumzia (Kobe), na ninaona nyuso zenye huzuni. Endapo Marekani na dunia itaridhia kunipa fungu langu, nitamfufua mtu huyu na bintiye,” ameeleza nabii huyo.
Aidha, amesema utajiri wa nyota huyo wa kikapu ni $ 500 milioni (Tsh 1.2 trilioni) na endapo familia yake itaridhia kumpa asilimia 10 ya utajiri huo, Tsh 115 bilioni atafanikisha hilo. Ila ametahadharisha kuwa ufufuaji huo hauwezi kukamilika pasi na kiwango hicho cha fedha kutolewa.
Amewataka waumini wake kumshukuru Mungu kwa kumteua yeye kufanikisha hilo, huku akiwaonya kuwa atakayepuuzia maneno yake atakumbana na balaa kubwa.
Kobe Bryant na Gianna ni miongoni mwa watu tisa waliofariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka na kuwaka moto, ajali iliyotokea jijini Los Angeles, Marekani, Januari 26 mwaka huu.
Watu hao walikuwa wakielekea katika mchezo wa mpira wa kikapu ambao Gianna alikuwa miongoni mwa wachezaji, na baba yake akiwa ndiye mkufunzi.