Kampuni ya mitindo ya mavazi inayomiliki chapa ya Adidas imeingia mkataba wa matangazo ya mitindo ya mavazi na Mwanamitindo kutoka Tanzania, Zuhura Bedel Said maarufu Zara
Zara anayetoka Zanzibar ameingia mkataba huo hivi karibuni baada ya kuwepo kwenye kumi bora, ambapo ataitangaza chapa ya Adidas kupitia mitindo ya mavazi.
Wanamitindo wengine tisa wanatoka katika jiji la Milano nchini Italia, jiji linalofahamika sana kwa mitindo ya mavazi kutokana na kuwepo kwa kampuni kubwa za mitindo kama Gucci, Valentino na Armani.
Akizungumza kwa njia ya simu na TBCOnline, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo amesema, mafanikio ya Tanzania kuendelea kutambulika Kimataifa na kupewa hadhi kama aliyopata Zara ni kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuitangaza nchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo filamu ya Tanzania The Royal Tour.
Amesema juhudi hizo za Rais Samia zimerahisisha kazi za Mabalozi kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.