Serikali ya Hong Kong imemuachia huru mwanaharakati wa Demokarsia na haki za binaadamu Joshua Wong baada ya kukamilisha kutumikia kifungo cha miezi miwili jela.
Joshua ambaye ameachiliwa huru mapema leo hii, alihukumiwa kutumikia kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kuandaa na kushiriki maandamano ya kudai kuboreshwa kwa hali ya demokrasia huko Hong Kong mwaka 2014.
Mara baada ya kuchia huru kutoka jela ya Lai Chi Kok, mwanaharakati huyo ameahidi kuwaunga mkono waandamanaji wanaopinga mswada wa serikali ya Hong Kong inayohusu kusafirisha watuhumiwa mbalimbali kwenda kusikiliza mashauri yao katika mahakama za China,ambapo tayari muswada huo umesitishwa.
Pia Joshua ambaye ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka ishirini na miwili, amesema waandamanaji wanapaswa kuendeleza maandamano ya kushinikiza kujiuzulu kwa mtendaji mkuu wa Hong Kong Carrie Lam, na kutaka kufutwa kabisa kwa muswada wa kusafirisha watuhumiwa kwenda kushitakiwa nchini China.
