Mwanafunzi mwenye umri mkubwa zaidi afariki

0
232

Priscilla Sitienei (Gogo), raia wa Kenya
ambaye anatajwa kuwa ni mtu aliyeanza elimu ya msingi akiwa na umri mkubwa zaidi kuliko watu wote dunia amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.

Gogo kama alivyokuwa akifahamika sana, neno ambalo maana yake ni Bibi kwa kabila la Kalenjin, alianza darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka 98.

Mjukuu wa Bibi huyo Sammy Chepsiror amesema bibi yake amefariki dunia kutokana na maradhi ya uzee na kwamba wanashukuru kwa maisha yake kwa kuwa ameipatia umaarufu mkubwa familia yao hasa baada ya hatua yake ya kuanza shule akiwa na umri mkubwa na hivyo kumfanya ajulikane na watu wengi duniani.

Wakati wa uhai wake, Bibi Priscilla Sitienei alisema ameamua kuanza shule akiwa na umri mkubwa tofauti na ilivyozoeleka
kwa kuwa anataka kujua kutumia simu na anataka kujua kusoma maandiko ya Biblia.

Alisema alishindwa kuanza shule akiwa mdogo kutokana na kukosa ada na kwamba hatua yake hiyo pia ina lengo la kuwahamasisha watoto ambao wameacha shule nchini Kenya kutokana na sababu mbalimbali kurejea shuleni na kuendelea na masomo yao.

Bibi huyo aliamua kuanza shule ya msingi baada ya kufanya kazi kama Mkunga wa Jadi kwa miongo kadhaa.