Mtu anayetuhumiwa kusababisha moto ulioteketeza jengo la ofisi za Bunge la Afrika Kusini zilizopo mjini Cape Town, Zandile Mafe leo amefikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Mafe anayedaiwa kukutwa na vitu vya milipuko amefikishwa mahakamani huku kukiwa na hali ya kurushiana lawama kuhusu tukio hilo, ambapo wakosoaji wamesema uzembe katika masuala ya ulinzi umetoa mwanya wa kutokea kwa moto huo.
Wakosoaji hao wamesema ulinzi ulikuwa dhaifu ambapo pia kamera za usalama hazikuwa zikifanya kazi, suala ambalo limepingwa na kukanushwa na Waziri mwenye dhamana ya Kazi na Miundombinu nchini Afrika Kusini Patricia De Lille na Spika wa Bunge la nchi hiyo Nosiviwe Mapisa Nqakula.
Moto huo ambao umeteketeza sehemu kubwa ya jengo la ofisi za bunge hilo ambalo ni la kihistoria nchini Afrika Kusini umedhibitiwa, huku maafisa wakiendelea na uchunguzi kubaini hasara iliyopatikana kutokana na sakata hilo.
Kesi ya Mafe imeahirishwa hadi tarehe 11 mwezi huu.