Takwimu za UNAids zinaonesha kuwa mwaka 2021 mtu mmoja alifariki dunia kila dakika kutokana na magonjwa yanayohusiana na upungufu wa kinga mwilini (Aids).
Taasisi hiyo imekadiria kuwa kila dakika mbili mwaka 2021, msichana au binti aliambukizwa Virusi vya UKIMWI.
Ripoti iliyopewa jina In Danger imewekwa wazi katika mkutano mkuu wa UNAids nchini Canada ambapo inaonesha zaidi kuwa wasichana na wanawake duniani wanajumuisha 49% ya maambukizi mapya mwaka 2021.
Hata hivyo, Kusini mwa Jangwa la Sahara kundi hilo lilikuwa ni 63% ya maambukizi mapya katika mwaka huo.
Zaidi ya watu milioni 1.5 walipata maambukizi ya Virus vya UKIMWI mwaka jana na takwimu zinaonesha kwamba maambukizi yanaongezeka.
Jumla ya watu milioni 38.4 wanaishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI duniani kote, ambapo Mashariki na Kusini mwa Afrika kuna idadi kubwa zaidi ambapo zaidi ya nusu ya mwenye maambukizi (milioni 20.6) wanaishi katika ukanda huo.