Msumbiji yataka mazungumzo na Wanamgambo

0
672

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema kuwa, milango ya mazungumzo iko wazi kwa Wanamgambo ambao wamekua wakifanya mashambulio katika jimbo la Cabo lililopo Kaskazini mwa nchi hiyo.

Wanamgambo hao wanaojulikana kama Al-Shabaab ambao hata hivyo inasemekana hawana uhusiano wowote na wale wa nchini Somalia, wamekuwa wakifanya mashambulio dhidi ya vikosi vya serikali pamoja na Raia tangu mwaka 2017.


Hadi sasa Wanamgambo hao wamefanya mauaji ya watu zaidi ya Mia Mbili pamoja na kuchoma moto nyumba zaidi ya Mia Sita katika jimbo hilo la Cabo.

Rais Nyusi amesema kuwa, lengo la serikali ya Msumbiji ni kuonana ana kwa ana na kufanya mazungumzo na Wanamgambo hao ili kufahamu wanahitaji nini, kwa
kuwa mpaka sasa hawafahamiki ni watu wa aina gani.

Kauli hiyo ya Rais Nyusi ya kutaka kufanya mazungumzo na Wanamgambo hao wa Al-Shabaab wa nchini Msumbiji, imekuja katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo
inatarajia kufanya uchaguzi Mkuu Oktoba 15 mwaka huu, ambapo kumekua na wasiwasi kuwa huenda wakafanya mashambulio zaidi wakati huo wa uchaguzi.

Mbali na jimbo la Cabo, Wanamgambo hao wamekua wakifanya mashambulio katika majimbo mengine ya Macomia, Palma na Nangade.