Mwalimu Peter Tabichi kutoka nchini Kenya, aliyeshinda Tuzo ya Mwalimu Bora Duniani mwezi Machi mwaka huu, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani katika Ikulu ya nchi hiyo.
Mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Trump, Mwalimu huyo pia anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani.
Peter Tabichi ambaye ni Mwalimu wa somo la Sayansi na Mtawa kutoka Shirika la Kikatoliki la Mtakatifu Fransisco wa Kapuchini, ameshinda tuzo hiyo ya Mwalimu Bora Duniani baada ya kuwashinda washiriki wengine Elfu Kumi waliochaguliwa kutoka nchi 179.
Akizungumzia tuzo hiyo, Mwalimu Tabichi amesema kuwa, anatamani kila mtoto afikie ndoto yake na ndio maana katika mshahara wake wa kila mwezi, amekua akitoa asilimia Themanini ya mshahara huo kusaidia Watoto wanaotoka kwenye familia zisizojiweza kujipatia mahitaji mbalimbali ya shule.
Akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Keriko iliyopo katika jimbo la Nakuru, Tabichi amesema kuwa, kazi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitabu na upungufu ya Walimu.