Moto wazuka chumba cha wagonjwa mahututi

0
188

Wagonjwa 13 waliokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Vijay Vallabh iliyopo kwenye jimbo la Maharashtra nchini India wamefariki dunia, baada ya moto kuzuka katika chumba cha wagonjwa mahututi wa corona.

Moto huo uliozuka majira ya alfajiri hii leo, pia umejeruhi wagonjwa wengine wanne ambao tayari wamehamishiwa katika hospitai nyingine.

Tukio hilo la moto limetokea katika kipindi hiki ambacho India inakabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa corona, huku hospitali nyingi zikiwa hazina oksijeni kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa aina hiyo.

Mpaka sasa haijafahamika sababu za kuzuka kwa moto katika chumba hicho cha wagonjwa mahututi, na uongozi wa jimbo hilo la Maharashtra umeagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina.

Kufuatia tukio hilo, Waziri Mkuu wa India, – Narendra Modi ametuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wagonjwa waliofariki dunia.