Moto wazua taharuki DRC

0
1590

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) imesema kuwa uharibifu uliotokea baada ya kuteketea kwa moto kwa  majengo yanayotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi  katika  Jamhuri hiyo ni mkubwa.

Waziri wa wizara hiyo Henri Sakanyi amesema kuwa majengo hayo yaliyopo katika mji wa Kinshasa  yameteketea kwa moto majira ya usiku na kuzua taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa mji huo.

Sakanyi amesema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na kwamba majengo yaliyoathirika zaidi ni yale ambayo yamekua yakitumiwa kuhifadhi vifaa vya uchaguzi.

Habari zaidi kutoka katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinasema kuwa takribani mashine Elfu Saba zilizotarajiwa kutumika wakati wa zoezi la upigaji kura zimeharibiwa na moto huo.

Tukio hilo la kwa kuteketea kwa moto kwa  majengo yanayotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi  katika  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limetokea zikiwa zimesalia siku Kumi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika Jamhuri hiyo, uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi  ya DRC kupitia kwa Msemaji wake  Jean Pierre Kalamba imeelezea matumaini yake kuwa tukio hilo halitavuruga mchakato wa uchaguzi.