Moto waendelea kuitesa California

0
1610

Uongozi wa jimbo la California nchini Marekani umethibitisha kuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na moto wa msituni imefikia 31 huku wengine zaidi ya mia mbili wakiwa hawajulikani walipo.

Maelfu ya watu katika jimbo hilo la California wamelazimika kuyakimbia makazi yao baada ya nyumba nyingi kuteketea kwa moto huo.

Habari zaidi kutoka katika jimbo hilo zinasema kuwa baadhi ya watu waliokufa, wamekufa wakiwa ndani ya magari yao walipokuwa wakijaribu kuukimbia moto huo.

Vikosi vya zimamoto katika jimbo la California vimesema kuwa kazi ya kuuzima moto huo wa msituni ni ngumu na haijawahi kutokea katika historia ya jimbo hilo.

Wamesema kuwa inaweza ikachukua muda wa wiki nzima ili kuweza kuuzima moto huo ambao unaendelea kuathiri uoto wa asili pamoja na makazi ya watu.

Upepo mkali na ukame vimetajwa kuwa ni moja kati ya vitu vinavyochochea moto huo wa msituni katika jimbo la California.