Mkuu wa Majeshi awafariji wafiwa Njombe

0
922

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vitahakikisha mauaji yanayosababishwa na imani potofu nchini yanakomeshwa.

Jenerali Mabeyo ametoa kauli hiyo mara baada ya kuwasili mkoani Njombe, mkoa ambao katika siku za hivi karibuni yametokea matukio ya mauaji ya watoto yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Tayari Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi amekutana na Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya wilaya zote za mkoa wa Njombe na ile ya mkoa huo, kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali yenye lengo la kukomesha mauaji hayo ya watoto.

Kwa upande wa Wakazi wa mkoa wa Njombe, Jenerali Mabeyo amewataka kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kama kawaida kwa kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vipo imara katika kutekeleza jukumu la kulinda raia na mali zao.

Akiwa mkoani Njombe, Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, amezifariji familia ambazo watoto wao wamekufa katika mauaji hayo.