Mke wa Mwanamfalme afunguka kuhusu ubaguzi wa rangi

0
283

Kashfa nzito imeikumba familia ya Kifalme ya Uingereza ambapo Meghan Markel, mke wa Mwanamfalme wa Uingereza (Prince Harry), amesema amekuwa akibaguliwa kutokana na rangi yake, hatua iliyomfanya kufikia wakati kutamani kujiua.

Akizungumza katika mahojiano na Oprah Winfrey, Bi. Markel amesema akiwa mjamzito kulikuwa na hofu kuhusu kwa kiasi gani mwanaye atakuwa mweusi, na hofu hiyo imechangia mtoto huyo kutopewa hadhi ya mwanamfalme.

Bi. Markel ambaye mama yake ni mweusi na baba yake ni mweupe amesema alikuwa na shauku kabla ya kuingia kwenye familia hiyo mwaka 2018, lakini alipoingia aliishia kuwa na mawazo ya kujidhuru/kujiua, baada ya kuomba msaada lakini hakupata.

Hata hivyo alikataa kueleza nani ndani ya Kasri la Kifalme alikuwa akizungumzia ubaguzi huo.

Wanandoa hao, Meghan na Prince Harry hawatekelezi majukumu yao katika familia ya kifalme na sasa wanaishi California nchini Marekani.