Misaada mbalimbali imeendelea kutolewa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi na tetemeko la chini ya bahari – Tsunami nchini Indonesia.
Misaada hiyo ambayo ni pamoja na ile ya chakula, maji na mafuta ya kula inasambazwa na wafanyakazi wa kutoa msaada ambao wamekua wakisindikizwa na vikosi vya ulinzi na usalama.
Taarifa kutoka nchini Indonesia zinasema kuwa zaidi ya watu elfu moja na mia tatu wamethibitika kufa hadi sasa, na idadi ya waliokufa itaendelea kuongezeka.
Tetemeko lenye ukubwa wa 7.5 kwenye vipimo vya matetemeko ya ardhi – Richta lilikipiga kisiwa cha Sulawesi na kusababisha tetemeko jingine chini ya bahari katika pwani ya mji wa Palu.
Ofisi ya shirika la msalaba mwekundu nchini Indonesia imesema kuwa miili 34 ya wanafunzi imepatikana katika kanisa moja ikiwa imefukiwa na kifusi.
Wanafunzi hao ni miongoni mwa wanafunzi 86 walioripotiwa kuwa hawajulikani walipo katika shule ya biblia ya Jonooge iliyopo katika kanisa hilo na kwamba hadi sasa wanafunzi wengine 52 hawajulikani walipo.