Mhalifu sugu nchini Ufaransa ambaye alitoroka gerezani akitumia helikopta iliyokuwa imetekwa nyara Redoine Faid, amekamatwa tena na polisi.
Faid aliyekua akitafutwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Ufaransa, amekamatwa kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Paris akiwa na ndugu yake na watu wengine wawili.
Kwa mara ya mwisho, wanaume watatu walimtorosha Faid kutoka gereza moja huko Reau na kumuingiza kwenye helikopta iliyokua ikiendeshwa na rubani aliyekuwa ametekwa nyara.
Mara kwa mara, mhalifu huyo mwenye umri wa miaka 46 amekua akijinasibu kuwa ni shabiki wa filamu za uhalifu za Hollywood kama vile Al Pacino thriller Scarface ambazo zimechangia mfumo wa maisha yake kwa kumfundisha namna ya kufanya uvamizi.
Mwaka 2013 alitoroka gerezani mara tu baada ya kufikishwa katika gereza hilo huku akitumia vilipuzi kulipua milango mitano ya gereza na kuwashika walinzi mateka na kuwatumia kama ngao.
Umaarufu wa Faid umechangiwa na kitabu chake alichokiandika mwaka 2009, kitabu kinachosimulia maisha yake akiwa mdogo kwenye mitaa ya Paris na kuibuka kuwa mhalifu.