Mgonjwa wa Ebola Atoroka

0
223

Mgonjwa mmoja wa Ebola ameripotiwa kutoroka katika kambi maalum ya matibabu ya  wagonjwa hao huko Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kuzua hofu ya kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo  uliosababisha vifo vya mamia ya watu huko DRC.

Taarifa za kutoroka kwa mgojwa huyo zilizotolewa na maofisa wa Afya katika jimbo la Kivu kaskazini, zinasema kuwa mgonjwa huyo ametoroka jana jioni kutoka katika kambi hiyo na kuhofu kuwa, mgonjwa huyo atakuwa amerejea katika jamii na kuhatarisha juhudi za kuzuia maambukizi mapya ya Ebola.

Maofisa hao wameongeza kuwa mtu huyo aligundulika kuwa na ugonjwa huo takribani siku tano zilizopita, msako wa kumtafuta mgonjwa huyo unaendelea kufanyika.

Mapema mwaka uliopita wa 2018 wagonjwa watatu wa Ebola walitoroka katika kambi maalumu ya matibabu ya wagonjwa wa Ebola iliopo magharibi mwa DRC kusababisha ongezeko la maambukizi ya Ugonjwa huo.