Mchungaji mwingine akamatwa kwa vifo vya waumini

0
222

Mchungaji Ezekiel Odero wa Kanisa la New Life International, Kenya amekamatwa na polisi kwa kuhusishwa na kesi ya Mchungaji Paul Mckenzie ya waumini waliofunga hadi kufa ili wawahi kufika mbinguni.

Kamanda wa Polisi Pwani, Rhoda Onyancha amesema uchunguzi umefanywa na kuonesha kuwa wawili hao wanaushirikiano katika vifo hivyo na kuwa upelelezi bado unaendelea juu ya kesi hiyo.

“Leo asubuhi tumemkamata Mchungaji Ezekiel Odero kwa tuhuma za vifo ambavyo vimekuwa vikitokea katika eneo lake na kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari,” amesema Onyancha.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa nyumba ya kuhifadhi maiti, Milele Funeral Home, Johnson Amani Kea, amethibitisha kuwepo kwa miili hiyo hapo.

“Hatukuwasilisha malalamiko. Polisi wanaendelea na mchakato wa kurekodi taarifa za miili mingapi ambayo tumeshughulikia hadi sasa kutoka kanisa la Mchungaji Ezekiel,” amesema Amani.

Aidha, kanisa la mchungaji huyo limefungwa kwa sasa.