Mbivu na Mbichi Kenya kujulikana leo

0
442

Muda mchache umesalia kabla ya Mahakama ya Juu ya Milimani ya Kenya kutoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Agosti 9 mwaka, na kumpa ushindi William Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza.

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya Urais ilifunguliwa na Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja na mgombea mwenza wake Martha Karua.

Raila na Karua wamefungua kesi hiyo ya kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa Agosti 15 mwaka huu na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) Wafula Chebukati, huku wakidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa uchaguzi huo, hivyo matokeo hayo ya Urais ni batili.

Uamuzi wa kesi hiyo utakaotolewa na jopo la Majaji saba wa mahakama ya Juu ya Milimani ya Kenya, ndio utatoa
mwelekeo kama Rais Mteule William Ruto ataapishwa tarehe 13 mwezi huu kuwa Rais wa Taifa hilo au Raila Odinga atapata fursa nyingine ya kuwania kiti cha Urais endapo matokeo ya Urais yatabatilishwa.