May kuungana na viongozi wa EU

0
1653

Waziri Mkuu wa Uingereza, -Theresa May anatarajiwa kuungana na viongozi wa nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) huko Brussels nchini Ubelgiji kuhudhuria mkutano maalum wa kilele wa viongozi hao.

Akiwa Brussels , pamoja na mambo mengine, May anararajiwa kuwashawishi viongozi hao wa nchi Wanachama wa EU kulegeza msimamo wao kuhusu mchakato wa Uingereza wa kujiondoa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.

May anaungana na viongozi hao zikiwa zimepita saa kadhaa baada ya kunusurika katika kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wabunge wa chama chake cha Conservative baada ya kupata kura 200 dhidi ya 117.

Wabunge hao 200 wamepiga kura ya kumuunga mkono May ili aendelee kuwa kiongozi wa chama hicho  na Waziri Mkuu wa Uingereza.

Hata hivyo hali hiyo inamaanisha kuwa May amepoteza uungwaji mkono wa theluthi moja ya Wabunge kutoka chama chake na hivyo kuashiria bado anakabiliwa na changamoto kubwa katika kutekeleza mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza wa kujiondoa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Kabla ya kura hiyo, May aliwaahidi wabunge wa chama chake cha Conservative kuwa hatawania tena muhula mwingine wa kukiongoza chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022.

Kwa sasa May hawezi kukabiliwa na kura nyingine ya kutokuwa na imani naye kutoka kwenye chama chake kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini iwapo atashindwa katika kura ya wabunge wote 650 wa Uingereza mwezi Januari mwaka 2019, serikali yake inaweza kukabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye.