Safari za ndege za Shirika la ndege la Kenya, leo zimevurugika kutokana na mgomo wa marubani wa shirika hilo, ambao wanashinikiza uwepo wa mazingira bora ya kazi.
Waziri wa Usafirishaji wa Kenya, Kipchumba Murkomen amesema, mgomo huo umesababisha ndege kadhaa kushindwa kufanya safari zake, hali ambayo imeathiri maelfu ya abiria.
Murkomen amewaambia waandishi wa habari jijini Nairobi kuwa hakukuwa na sababu za msingi kwa marubani hao kufanya mgomo na kwamba kitendo likichofanyika ni sawa na uhujumu uchumi.
Marubani hao wamedai kuwa Shirika la Ndege la Kenya limeshindwa kushughulikia malipo yao na pia limeshindwa kuchangia
michango ya kila mwezi ya pensheni kwa wafanyikazi.
Malipo hayo yote yamefikia shilingi bilioni 6.5 za Kenya.
Shirika la Ndege la Kenya, ambalo linamilikiwa kwa asilimia fulani na serikali ya Kenya, ni moja ya mashrika makubwa zaidi ya usafiri wa anga barani Afrika.
Licha ya shirika hilo kutoa huduma ya kuziunganisha nchi nyingi za Afrika, Ulaya na Asia, limekuwa likikabiliwa na misukosuko ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kujiendesha kwa hasara kwa miaka kadhaa.