Marekani yazuia safari zote kutoka Ulaya

0
654

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kuzuia safari zote kutoka Ulaya kuingia nchini humo, ikiwa ni moja ya njia za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Katika hotuba yake kwa Taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni, Trump amesema kuwa safari zote kutoka Ulaya kwenda nchini Marekani  zitazuiwa kwa muda wa siku 30 zijazo kuanzia siku ya Ijumaa usiku ili kuzuia maambukizi mapya.

Hata hivyo Rais Trump amesema kuwa uamuzi huo ambao ameuita kuwa ni mgumu na muhimu hautaihusisha nchi ya Uingereza ambayo ina watu 460 waliothibitika kuwa na virusi vya corona.

Zaidi ya watu elfu moja wamethibitika kuambukizwa virusi vya corona nchini Marekani, huku wengine 38 wakiripotiwa kufariki dunia.

Katika hotuba hiyo Rais Trump ameushutumu Umoja wa Ulaya kwa  kushindwa kuchukua hatua zaidi za kukabiliana na maambukizi ya corona kama ambavyo zimechukuliwa na Marekani.

Pia ametangaza kutoa mkopo wa mabilioni ya dola za kimarekani kwa wafanyabiashara wadogo wa nchi hiyo na kutoa nafuu ya kodi kwa wafanyabishara wote ili waweze kukabiliana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na mlipuko wa  virusi hivyo vya corona.