Marekani na Kenya kukuza biashara

0
2958

Rais Donald Trump wa Marekani amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya mjini Washington na kugusia zaidi masuala ya biashara na usalama.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imesema kuwa akiwa katika ziara yake ya siku nne nchini Marekani, Rais Kenyatta na Rais Trump wamekubaliana na kutangaza mikataba ya jumla ya dola milioni 900 za Kimarekani.

Rais Kenyatta ni kiongozi wa tatu kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara kukaribishwa Ikulu ya Marekani na kufanya mazungumzo na Rais Trump.

Akizungmza mara baada ya mazunguzo yake na Rais Trump, Rais Kenyatta amesema kuwa Kenya imekuwa na ushirikiano mzuri na wa kipekee na Marekani katika masuala ya ulinzi na usalama hasa katika vita dhidi ya ugaidi na kinachofanyika hivi sasa ni kuimarisha uhusiano katika masuala ya biashara pamoja na uwekezaji.

Kwa upande wake Rais Trump ameelezea kufurahishwa na pendekezo lililowasilishwa na kampuni ya ujenzi kutoka nchini Marekani, – Bechtel Corporation la kutaka kupewa kandarasi ya ujenzi wa barabara ya kisasa ya kutoka Nairobi kwenda Mombasa nchini Kenya ambapo mataifa hayo mawili yamekubaliana kuendelea na majadiliano zaidi ili kuafikiana kuhusu ufadhili wa ujenzi huo.