Makubaliano ya Korea Kaskazini na Korea Kusini yaungwa mkono

0
2187

Rais Donald Trump wa Marekani ameunga mkono makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini katika mkutano wao uliofanyika mjini Pyongyang.

Trump amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi hao kuhusu Korea Kaskazini ni hatua nzuri kwa kuwa awali ilionekana kama Marekani na nchi hiyo zitaingia katika mgogoro kutokana na mpango wake wa nyuklia.

“Tumerejeshewa wafungwa wetu, tunarejeshewa mabaki ya wapiganaji wetu,lakini la muhimu hakuna tena majaribio ya makombora, majaribio ya silaha za nyuklia na sasa wanataka kuomba kuandaa mashindano ya olimpiki, tuna mambo mengi mazuri yanayoendelea,” amesema Rais Trump.

Rais huyo wa Marekani amerejea kauli yake kuwa utawala wake umekuwa chachu ya kuleta mazingira tulivu yanayoonekana hivi sasa.

”Kumbuka hili, kabla ya kuwa rais watu wengi walifikiri kuwa tunakwenda vitani lakini sasa mahusiano mazuri yamejengwa, nawaambia kwa mawazo yangu, mahusiano ni mazuri, hali imekuwa ya utulivu, kwa sasa tunapoongea hali imetulia, amekuwa mtulivu, nimekuwa mtulivu hivyo tutaona mambo yatakavyokuwa” ameongeza Rais Trump.

Hivi karibuni Rais Kim Jong-un wa Korea Kaskazini alikutana na mwenzake wa Korea Kusini, – Moon Jae-in katika mji wa Pyongyang, mkutano ambao ni wa tatu kwa viongozi hao.
Wakati wa mkutano huo Kim alitangaza kuzima moja ya mitambo yake mikubwa ya nyuklia na majaribio ya makombora wa Tongchang-ri, tukio litakaloshuhudiwa na wataalam wa nyuklia kutoka mataifa mbalimbali.