Imezoeleka wanawake wengi hubeba mikoba kwa madhumuni ya mapambo, au kuongeza mwonekano mzuri kutokana na vile ambavyo wamevaa kwa siku hiyo.
Hii ni tofauti kwa Malkia Elizabeth II, ambaye yeye alipochagua kutoka na kwenda mahali na moja ya mikoba yake yenye rangi nzuri, alifanya kwa kusudi maalum.
Kwa kila mkoba alioubeba Malkia Elizabeth II, kazi kubwa alikuwa akiutumia kwa dhumuni la kufanya mawasiliano na wasaidizi wake.
Wasaidizi hao aliokuwa akiwasiliana nao ni pamoja na wale wa Ikulu ama wale wa familia ya kifalme.
Mawasiliano hayo yalikuwa hasa ya ishara
ambapo alikuwa akiuvaa mkoba huo kwa ishara tofauti tofauti, na hapo wasaidizi wake walielewa kwa muda huo anahitaji kitu gani.
Kwa mfano kama alikuwa anashiriki kwenye shughuli fulani akawa amechoka na anahitaii kurudi kupumzika, aliweza kubadilisha mkoba katika mkono wake wa kulia na kuupeleka mkono kushoto, hapo wasaidizi wake walielewa sasa anahitaji kwenda kupumzika.
Na alipotoa ishara ya aina hiyo, iliwalazimu wasaidizi wa Malkia Elizabeth II haraka kuangalia namna ya kumuonda katika eneo hilo bila kuchelewa pindi shughuli aliyokua akihudhuria ama mkutano unapomalizika.
Vilevile ikiwa alikuwa kwenye mazungumzo na akaupiga mkoba wake chini, ni ishara kwamba amechoshwa na tukio linaloendele na anataka limalizike.
Na alipokuwa akiutupa mkoba wake sakafuni muda yuko mezani ni ishara kwamba amechoshwa na hafla ya chakula cha jioni hivyo anataka hafla hiyo isichukue zaidi ya dakika tano mbele.
Lilikuwa ni jambo la kawaida kwa Malkia Elizabeth II kutumia ishara, unaweza ukajiuliza kwa nini alipendelea kutumia mikoba yake kama njia ya mawasiliano badala ya kuongea.
Jibu ni kwamba, unapozaliwa ndani ya familia ya kifalme, kuna sheria walizojiwekea na taratibu ambazo huna budi kuzifuata.