Majaji wafukuzwa kazi kwa tuhuma za rushwa

0
1303

Rais Nana Akufo-Addo  wa Ghana amewafukuza kazi Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo, ikiwa ni miaka mitatu baada ya tume iliyoundwa kuchunguza vitendo vya rushwa kutoa ripoti yake na kuwatuhumu kuwa walihusika na vitendo hivyo.

Mbali na kuwafukuza kazi majaji hao, Rais Akufo-Addo pia amekabidhi majina ya majaji hao kwa jeshi la polisi la Ghana ili liendelee na upelelezi zaidi na baadae kuwafungulia mashitaka.

Hata hivyo  haijafahamika ni kwa nini Rais  Akufo-Addo ameamua kuchukua uamuzi hivi sasa, baada ya kupita miaka mitatu tangu kutolewa kwa ripoti hiyo.

Majaji hao watatu wa Mahakama Kuu ya Ghana ni miongoni mwa zaidi ya watumishi mia moja wa idara ya mahakama ya nchi hiyo walioorodheshwa katika ripoti ya watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ripoti iliyoitikisa nchi hiyo mwaka 2015.

Tayari majaji hao wamefungua shauri katika mahakama ya Jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ili kupinga hatua hiyo ya kufukuzwa kazi na pia wameelezea kusikitishwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Rais  Nana Akufo-Addo.

Mwandishi wa habari za uchunguzi wa Ghana, – Anas Aremeyaw Anas ndiye aliyefichua taarifa za watumishi wa idara mbalimbali nchini humo ikiwemo ile ya mahakama kuhusika na vitendo vya rushwa ambapo aliwarekodi watumishi hao wakichukua rushwa hizo kwa njia mbalimbali.