Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amewaruhusu zaidi ya Madaktari Mia Nne nchini humo ambao walifukuzwa kazi kwa kushiriki katika mgomo, kurejea kazini katika
kipindi cha saa 48 pasipo kuomba upya ajira zao.
Rais Mnangagwa ametangaza uamuzi huo Mjini Harare, saa chache baada ya kukutana na viongozi wa Makanisa nchini humo, na hivyo kubatilisha uamuzi wa awali uliosema kuwa
Madaktari hao hawatarejea kazini mpaka hapo watakapotuma maombi ya ajira.
Madaktari hao zaidi ya Mia Nne nchini Zimbabwe walipewa barua za kufukuzwa kazi kutokana na kushiriki katika mgomo wa kudai nyongeza ya mishahara.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, madaktari hao waligoma kufanya kazi, na kushinikiza kupatiwa nyongeza hiyo ya mishahara, huku pia wakilalamikia mazingira magumu ya kufanyia kazi.