Korea Kaskazini yashutumiwa kutumia Drone kushambulia Kusini

0
143

Maafisa wa jeshi la Korea Kusini wanasema Korea Kaskazini imerusha ndege kadhaa zisizo na rubani katika mpaka wao wa pande zote mbili.

“Ndege zisizo na rubani” zilikiuka anga ya Korea Kusini katika maeneo ya mpakani karibu na mkoa wa Gyeonggi, wamesema wakuu wa jeshi la nchi hiyo.

Moja ya ndege zisizo na rubani ziliruka hadi Mji Mkuu Seoul, kulingana na ripoti.

Jeshi la Korea Kusini limesema kuwa limefyatua risasi za onyo kabla ya kutuma ndege na helikopta kuziangusha ndege hizo.

Moja ya ndege za kivita, ndege nyepesi ya KA-1, imeanguka baadaye, lakini marubani wake wawili wamenusurika bila kujeruhiwa.

Ndege hiyo imeanguka katika Kaunti ya Hoengseong, mashariki mwa Seoul, mara baada ya kupaa kutoka kituo cha anga katika mji wa karibu wa Wonju, kulingana na jeshi la wanahewa, limenukuliwa na shirika la habari la Yonhap.

Korea Kusini pia imesimamisha ndege kupaa na kutua katika viwanja vyake vya Incheon na Gimpo kwa takribani saa moja.

Mara ya mwisho ndege isiyo na rubani ya Korea Kaskazini kuvuka mpaka ilikuwa miaka mitano iliyopita mnamo Juni 2017.