Korea Kaskazini yamuita makamu wa Trump ‘mpumbavu’, mkutano Juni 12 bado njiapanda

0
2034

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence (Picha na REUTERS)

Vita ya maneno inaendelea kati ya maofisa wa Korea Kaskazini na Marekani ambapo katika hatua ya hivi karibuni ofisa mmoja wa ngazi za juu katika serikali ya Korea Kaskazini Choe Son-hui amemuita Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence kuwa ni ‘mpumbavu’ kwa kuilinganisha nchi hiyo na Libya.

Ofisa huyo pia ametishia kuwepo tayari kwa Korea Kaskazini kwa vita ya nuklia iwapo diplomasia itashindwa, akisema kuwa nchi hiyo haiwezi kamwe kuibembeleza Marekani kumaliza mgogoro huo kidiplomasia na wala kujaribu kuishawishi ihudhurie mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu nchini Singapore.

Katika siku za karibuni pande zote mbili zimekuwa zikionya kwamba kuna hatari mazungumzo hayo ya Juni 12 yakasogezwa mbele au kufutwa kabisa, ambapo Pyongyang imesema haitahudhuria kama Marekani itasisitiza kuwa nchi hiyo iachane na nuklia huku Trump akisema juzi kuwa ni Korea Kaskazini inayopaswa kutimiza masharti ili mazungumzo hayo yaweze kufanyika kama ilivyopangwa.

Choe Son-hui, mwanamama ambaye katika muongo mmoja uliopita ameshiriki katika harakati mbali mbali za kidiplomasia na Marekani, amesema Pence ametoa kauli zisizoonyesha heshima kwa Korea Kaskazini, ikiwa ni pamoja na kusema kwamba nchi hiyo inaweza kuishia kama Libya.

Katika makala iIiyotangazwa na Shirika la Habari la Serikali ya Korea Kaskazini (KCNA), Choe Son-hui amesema Pence ni mjinga na mwanasiasa uchwara, kwa kuilinganisha nchi ya nuklia ya Korea Kaskazini na Libya ambayo ilikuwa na vifaa vichache tu tena ambavyo ‘ilivichezea’.

“Kama mtu niliyeshiriki sana mambo ya Marekani, siwezi kuficha mshangao wangu kuhusu kauli za kijinga na kipumbavu kutoka kwenye mdomo wa Makamu wa Rais wa Marekani” amesema Choe na kuongeza “Kama Marekani itakutana nasi katika chumba cha mkutano au katika uwanja wa vita vya nuklia, ni suala linalotegema kwa asilimia 100 katika uamuzi na mwenendo wa Marekani”.

Hivi karibuni mshauri wa usalama wa Marekani John Bolton pia aliiudhi Korea Kaskazini hadi ikatishia kujitoa katika mazungumzo yanayotarajiwa, baada ya kusema Korea Kaskazini inaweza kufuata mtindo uliotumika Libya kuiondolea uwezo wa kinuklia.

Wachambuzi wanasema kwa vile Choe Son-hui ni mtu mwenye nguvu katika siasa za Korea Kaskazini na mmoja wa wasaidizi wakuu wa Rais Kim jong-un, bila shaka kauli alizotoa zina baraka zote za Rais Kim mwenyewe.

Kwamba hadi sasa Pyongyang haijamrushia matusi Donald Trump ambaye kwa kiasi fulani juzi alitoa kauli zinazokaribia kufanana na za hao wasaidizi wake wa karibu, inaashiria kuwa huenda Korea Kaskazini bado haijachukua uamuzi wa kuyatupila mbali moja kwa moja, mazungumzo hayo.