Kiongozi wa Chama Cha Madaktari nchini Zimbabwe (ZHDA),-Dkt Peter Magombeyi ambaye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha siku chache zilizopita, amepatikana akiwa hai.
ZHDA imesema kuwa, licha ya kupatikana kwa Dkt Magombeyi, Wanachama wa chama hicho wataendelea na mgomo wao.
Dkt Magombeyi ambaye katika siku za hivi karibuni ameongoza mgomo kushinikiza Madaktari nchini Zimbabwe kupata nyongeza ya mshahara na kuboreshewa mazingira ya kazi, amepatikana umbali wa Kilomita Arobaini kutoka mji Mkuu wa nchi hiyo,- Harare na Polisi wamesema kuwa wanaendelea kuchunguza tukio hilo.
Akizungumza baada ya kupatikana, Dkt Magombeyi amesema kuwa, alitekwa na watu Watatu ambao walimpeleka hadi msituni na baada ya kumuachia, alitembea hadi kwenye duka alikokutwa na Askari.
Tayari Kiongozi huyo wa Chama Cha Madaktari nchini Zimbabwe amechukuliwa vipimo vya aina mbalimbali ili kujua hali ya afya yake.