Serikali ya Msumbiji imewaagiza watu walioko katika maeneo ya mabondeni na maeneo ya kati kwenda kwenye maeneo yenye miinuko ili kujiepusha na kimbunga Kenneth, ambacho licha ya kuipiga nchi hiyo, kinatarajiwa kurejea tena.
Baadhi ya watu katika eneo la Pemba nchini Msumbiji wamekimbilia katika kanisa moja ambalo viongozi wake wamefungua milango kuwapokea watu wanaokimbia kimbunga Kenneth, ambacho hadi sasa kimesababisha vifo vya watu 41.
Serikali ya Msumbiji imesema kuwa kimbunga Kenneth kinaweza kusababisha maafa zaidi, licha ya kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu, huku miti mikubwa nayo ikiwa imeng’olea na kutupwa mbali.
Baadhi ya watu wamekataa kuondoka katika nyumba zao na kwenda katika maeneo yenye miinuko kwa madai kuwa hawana mahali pa kwenda wala mahali pa usalama penye uhakika kwa ajili ya maisha yao.