Kimbunga Ian chaleta madhara Florida

0
155

Kimbunga Ian kimesababisha mafuriko makubwa katika jimbo la Florida nchini Marekani, ambapo miti na magari vimesombwa na maji.

Habari zaidi kutoka katika jimbo hilo zinaeleza kuwa, kimbunga Ian ambacho hapo jana kilitua katika pwani ya Florida pia kimeharibu nyumba kadhaa, huku watu milioni moja na nusu wakikosa huduma ya umeme katika jimbo hilo.

Kimbunga hicho cha Ian kimetajwa na wataalam wa hali ya hewa kama mojawapo ya dhoruba zenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Marekani.

Kituo cha vimbunga cha Marekani kimesema dhoruba hiyo ya kiwango cha nne,
Ilitua karibu na mji wa Cayo Costa
ikiwa na kasi ya kilomita 241 kwa saa.

Baada ya kimbunga Ian kusababisha mafuriko katika eneo kubwa la Florida, sasa inaelezwa kimeonyesha uelekeo wa kaskazini mashariki mwa penisula ya kaskazini Magharibi.

Awali uongozi wa jimbo la Florida pamoja na serikali ya Marekani walitoa tahadhari kwa wakazi wa maeneo yaliyolengwa na dhoruba hiyo, ambapo pia wakazi wengi walilazimika kuyahama makazi yao ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.