Kim na Trump tayari kwa mkutano

0
2080
Hoteli ya Capella iliyoko Singapore ambako mazungumzo kati ya Rais Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un watafanya mazungumzo yao kesho Jumanne

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimesema Kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un na Rais wa Marekani Donald Trump watajadili kuliondolea nuklia eneo la Peninsula ya Korea na namna ya kujenga mpango wa kuleta amani ya kudumu katika eneo hilo.

Kim na Trump wamewasili Singapore jana Jumapili wakijiandaa na mkutano wao utaofanyika kesho Jumanne katika hoteli ya Capella iliyoko kisiwa cha Sentosa, kuanzia saa tatu asubuhi,kwa saa za Singapore.

Huo utakuwa ni mkutano wa pekee kwa nchi hizo zenye uhasama wa kihistoria, ambapo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini walioko madarakani, kukutana uso kwa uso kwa mazungumzo.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 20 zitatumika kugharamia mkutano huo ikiwemo gharama za maofisa usalama wapatao 5000 ambao wapo nchini Singapore kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wakati wote wa mkutano huo.

Kwa mujibu wa maofisa wa utawala wa Rais Trump, baada ya viongozi hao kupeana mikono kwa mara ya kwanza na kupigwa picha na waandishi wa habari, wataanza mazungumzo yao wakiwa wawili tu na wakalimani wao.

Viongozi hao wawili wameonyesha kuwa na matumaini makubwa ya kuwa mazungumzo hayo yataleta manufaa, lakini baadhi ya wachambuzi wameeleza wasiwasi wao kuhusu kufikia muafaka, kwani inaonekana kuna tafsiri mbili tofauti kati ya pande hizo kuhusiana na kinachoitwa kuondoa nuklia katika eneo la peninsula ya Korea.

Korea Kaskazini wakati wote imekuwa ikitoa tafsiri pana ya jambo hilo na kutaka lihusishe hata vifaa vya kijeshi vya Marekani vilivyopo katika eneo hilo na ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini, ambao ‘umekuwa ukitishia amani katika eneo hilo’.

Kwa upande mwingine viongozi wa ngazi za juu wa Marekani wamewahi kunukuliwa wakisema wanachotaka wao ni kuiondolea nuklia Korea Kaskazini kama ilivyotokea kwa Libya au Irak.

Kwa mujibu wa wachambuzi kama anachofikiria Trump ni kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mkataba wowote wa aina hiyo bila kutoa majukumu kwa Korea Kusini au Marekani yenyewe, itakuwa ni ngumu mkutano huo kufanikiwa.