Rais wa Argentina Alberto Fernandez, ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa nchini humo kufuatia kifo cha gwiji wa soka duniani Diego Armando Maradona, aliyefariki kwa maradhi ya moyo akiwa nyumbani kwake mjini Tigre.
Rais Fernandez amesema Taifa lake limempoteza shujaa aliyeifanya Argentina kuwa juu na raia wake kujisikia fahari ambapo watamkumbuka kwa kazi yake nzuri aliyoifanya wakati wa uhai wake.
Maradona amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60, ambapo mapema mwezi huu alifanyiwa upasuaji wa ubongo ambao madaktari walimwambia ulifaulu.
Gwiji wa zamani wa soka Pele na nyota wa sasa wa Argentina Lionel Messi wamesema ni siku ya masikitiko kwa Argentina na familia ya soka ulimwenguni kote.
Mwaka 1986 akiwa nahodha wa kikosi cha timu ya Argentina, Maradona aliliongoza Taifa lake kushinda Kombe la Dunia nchini Mexico huku akionesha jitihada binafsi na uwezo mkubwa uliochangia Argentina kutwaa taji hilo.
Wakati akicheza soka la ushindani, Maradona aliwahi kuzitumikia klabu za Barcelona ya Hispania, na Napoli ya Italia ambapo Napoli alinyakua ubingwa wa ligi ya Serie A kwa misimu miwili.
Maradona aliifungia timu ya Taifa ya Argentina magoli 34 katika michezo 91, akishiriki michuano minne ya Kombe la Dunia.