Kenyatta awataka Wakenya kuendeleza umoja na mshikamano

0
464

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amewataka wananchi wote wa Taifa hilo kuendeleza umoja na mshikamano, ikiwa ni moja ya njia ya kumuenzi Rais wa Pili wa nchi hiyo Mzee Daniel arap Moi.

Rais Kenyatta ametoa wito huo alipowaongoza wananchi wa Kenya kutoa heshima zao ya  mwisho kwa mwili wa kiongozi huyo ambaye aliliongoza Taifa hilo kwa miaka 24 kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 2002.

Amesema kuwa, katika kipindi chote cha uongozi wake mzee Moi alikua akisisitiza mshikamano na umoja wa kitafa, hali iliyoifanya nchi hiyo kupata maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali.

Ametoa wito kwa viongozi wa ngazi zote nchini humo kuiga mambo yote aliyokua akiyafanya Mzee Moi katika kipindi cha uongozi wake, yaliyokua na lengo la kuhakikisha Taifa hilo linasonga mbele.

Mwili wa Rais huyo wa pili wa Kenya aliyefariki dunia Jumanne iliyopita,  utalala katika Bunge la nchi hiyo kwa muda wa siku tatu kabla ya kuagwa kitaifa Jumanne Februari 11.

Siku ya Jumatano mwili huo utapelekwa nyumbani kwake Kabarak kwa ajili ya mazishi ya kitaifa yatakayofanyika kwa heshima zote za kijeshi.

Mzee Moi anakua kiongozi wa pili aliyewahi kushika wadhifa wa Urais nchini Kenya kuagwa na kuzikwa kwa heshima zote za kijeshi na pia anakua kiongozi wa 6 nchini humo kufanyiwa mazishi ya aina hiyo tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 1963.

Rais Kenyatta ndiye alitangaza Mzee Moi afanyiwe mazishi ya aina hiyo na tayari ametangaza siku ya Jumatano yatakapofanyika mazishi rasmi ya Mzee Moi kuwa ni siku ya mapumziko.