Kenya yatakiwa kushughulikia tatizo la njaa

0
371

Raia wa Kenya wameendelea na kampeni yao katika mitandao mbalimbali ya kijamii inayojuliana kama WeCannotIgnore kwa lengo la kuihamasisha serikali kushughulikia tatizo la ukame na njaa linaloyakabili majimbo mbalimbali ya nchi hiyo.

Kampeni hiyo imeanzishwa baada ya kile kinachodaiwa kuwa serikali Kuu na zile za majimbo zimekua hazishughulikii kwa uzito suala hilo la ukame na njaa, huku baadhi ya viongozi wakikanusha jambo hilo.

Takribani majimbo kumi na matatu nchini Kenya yanakabiliwa na ukame na njaa,  kufuatia kutokuwepo kwa mvua za kutosha katika maeneo hayo.

Majimbo hayo ni Turkana, Baringo, Pokot Magharibi, Marsabit, Wajir, Kilifi, Tana River, Samburu, Makueni, Isiolo, Mandera, Kajiado, Kwale na Garissa.

Habari zaidi kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa majimbo ya Turkana, Pokot Magharibi na Marsabit ndio yameathirika zaidi na kusababisha hata vifo.

Licha ya habari hizo za njaa kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na hata kwenye vyombo vya habari, baadhi ya viongozi wa serikali ya Kenya wamekua wakikanusha kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa tayari serikali iliishatoa Shilingi Bilioni Mbili za nchi hiyo ikiwa ni za ziada,  kwa ajili ya kuwapatia chakula na maji wakazi wa majimbo hayo kumi na matatu yanayokabiliwa na ukame pamoja na njaa.