Kenya yasisitiza kuendeleza ushirikiano na Tanzania

0
171

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema nchi hiyo itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Kenya unaendelea kuimarika na kuwa na manufaa kwa Wananchi wa pande zote mbili.

Rais Kenyatta ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Nairobi wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye yupo nchini Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Amesema Kenya haiichukulii Tanzania kama nchi jirani tu, bali pia inaichukulia kama ndugu wa damu.

Rais Kenyatta amesisitiza kuwa mataifa hayo mawili yana historia ndefu na yanaunganishwa na mambo mengi yakiwemo ya kiutamaduni na lugha, hivyo vi vema yakaendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali.

Amesema mbali na suala la kuimarisha ushirikiano, wakati wa mazungumzo yao pia wamejadili namna ya kutatua changamoto za Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya ambao mara kadhaa wamekuwa wakikutana nazo hasa katika maeneo ya mpakani.

Kwa mujibu wa Rais Kenyatta, jambo jingine walilojadili ni namna ya kuboresha usafiri wa anga, barabara, reli na ule wa majini, lengo likiwa ni kukuza biashara na uwekezaji.