Kenya yaongeza muda wa kupata hati mpya za kusafiria

0
360

Serikali ya Kenya imeongeza muda wa miezi 12 zaidi ili kuwawezesha Raia wa nchi hiyo kupata hati za kusafiria kwa mfumo wa Kielektroniki.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imeeleza kuwa, kwa sasa hati za kusafiria za zamani zitaendelea kutumika hadi Machi Mosi mwaka 2021, na hivyo kuwawezesha takribani Raia Milioni Mbili wa nchi hiyo wengi wao wanaoishi nje ya nchi kupata hati hizo mpya za kusafiria.

Matumizi ya hati za kusafiria za zamani yalikua yafikie ukomo Septemba Mosi mwaka 2019, lakini Serikali ya Kenya ilisogeza mbele muda huo hadi Machi Mosi mwaka huu, na kufuatia tangazo hilo la hivi karibuni hati hizo zitafikia ukomo mwaka 2021.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya pia imeeleza kuwa, Serikali ya nchi hiyo imefungua vituo katika miji ya Dubai, Johannesburg nchini Afrika Kusini, Berlin, – Ujerumani , Paris nchini Ufaransa, London huko Uingereza na Washington nchini Marekani ili kuwawezesha Raia wa Kenya wanaoishi karibu na miji hiyo kupata hati zao mpya za kusafiria.