Kazi ya kuhesabu kura yaendelea Nigeria

0
698

Maafisa wa Tume ya Uchaguzi nchini Nigeria, wanaendelea kuhesabu kura kufuatia uchaguzi wa Rais uliofanyika Jumamosi Februari 23.

Kazi hiyo ya kuhesabu kura ilichelewa kuanza kutokana na kuongezwa muda wa kupiga kura katika baadhi ya majimbo, ambapo kura zilipigwa hadi usiku.

Katika kinyang’anyiro hicho, mpinzani mkubwa wa Rais Muhammadu Buhari mwenye umri wa miaka 76 ni Atiku Abubakar mwenye umri wa miaka 72, na ambaye ni Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia kesho Jumatatu.

Zaidi ya raia elfu 84 wa Nigeria walijiandikisha kupiga kura katika vituo takribani Laki Moja na Ishirini Elfu vilivyoandaliwa.

Awali uchaguzi huo wa Rais ulipangwa kufanyika Februari 16 mwaka huu, lakini uliahirishwa kwa muda wa wiki moja kutokana baadhi ya maandalizi kutokamilika.