Jaji nchini Kenya mbaroni kwa kushirikiana na mshtakiwa wa mauaji

0
429

Jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini Kenya amekamatwa kwa kudaiwa kumsaidia na mshtakiwa wa kesi ya mauaji ya mumewe.

Sankale ole Kantai alikamatwa Ijumaa, Februari 21 na kuachiwa kwa dhamana Februari 22, kwa kosa la kumsaidia mwanamama Sarah Wairimu katika kuandaa maelezo ya kuwapa polisi.

Mnamo Julai mwaka jana, mfanyabiashara mwenye asili ya Uholanzi, Tob Cohen aliyekuwa mume wa Wairimu alipotea na mwili wake ulipatikana Septemba, miezi miwili baadae nyumbani kwake Kitisuru ukiwa ndani ya matanki ya maji yaliyochimbiwa ardhini huku macho yakiwa yamezibwa, na mikono imefungwa.

Wairimu ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa kazi (personal assistant) wa Cohen alikataa mashtaka hayo ya mauaji katika kesi inayomkabili.

Cohen ambaye alihamia Kenya akiwa anafanya kazi kwenye kampuni ya Philips Afrika Mashariki na baadae kuanzisha kampuni binafsi alikutwa na mauti akiwa kwenye hatua za kushughulikia talaka, na siku nane kabla ya kifo chake aliandika barua kwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuelezea kuwa anahofia maisha yake.

Katika barua hiyo Cohen alieleza juu ya ndoa yake na kwamba mke wake hakuwa akimfanyia vitu vizuri na tayari alishamfungulia mashtaka ya mashambulizi dhidi yake.

Jaji Kantai anatarajiwa kurudi mahakamani mapema wiki ijayo kwa mashtaka ya kuipindua haki na kungilia mashahidi.